Twitter na umaarufu wa marais Wa Afrika

Image caption Rais Zuma wa Afrika Kusini

Siku hizi, takriban viongozi wote wanaonuia kupenya zaidi katika ulingo wa siasa wana akaunti katika mtandao wa Twitter, wakitaka sana maoni yao yasomwe na wengi.

Muda mfupi tu baada ya kutangazwa mshinidi katika uchaguzi wa urais nchini Marekani Novemba mwaka uliopita, Barack Obama alituma ujumbe mmoja mfupi akitumia Twitter: "Miaka mingine minne zaidi".

Ujumbe huo uliandamana na picha iliyomuonyesha yeye na mkewe wakikumbatiana.

Katika historia ya Twitter, ujumbe huu ndiyo umesomwa na watu wengi na kusambazwa zaidi.

Viongozi wa Afrika

Lakini umaarufu wa marais wa Afrika hauko katika kiwango cha Obama katika Twitter.

John Mahama wa Ghana ana watu 11,000 wanaomfuata, mara mbili ya idadi ya wale wa Alassane Ouattara, rais wa Ivory Coast.

Jakaya Kikwete wa Tanzania ana takriban wanaomfuata 50,000 huku Paul Kagame wa Rwanda ana karibu 104,000.

Jacob Zuma, rais wa Afrika kusini, anaongoza kwa kuwa na zaidi ya wafuasi 200,000 katika Twitter. Lakini kwa upande mwingine kabisa Rais Mwai Kibaki wa Kenya hana hata akaunti ya Twitter.

Ingawaje utumizi wa Twitter ulianza kama jukwaa la watu kubadilishana habari kuhusu starehe zao, sasa utumizi wake umebadilika na kuwa njia muhimu ya mawasiliano ya kila aina kwa wengi.

Wiki iliyopita Twitter ilitumika kama chombo kikuu cha kampeni za kufanya mabadiliko nchini Afrika Kusini kufuatia ubakaji na mauaji ya kinyama ya msichana wa miaka 17 nchini humo.