Kipindi cha lala salama Mali

Rais wa Ufaransa Francois Hollande, amesema kuwa majeshi ya nchi yake yako katika awamu ya mwisho ya mapambano dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu nchini Mali.

Alisema kuwa makabilinao makali yalitokea katika maeneo ya milimali ya Ifoghas ambako wapiganaji wa kiisilamu walikuwa wanajificha.

Bwana Hollande pia alisifu wanajeshi wa Chad kwa juhudi zao nchini humo.

Wanajeshi 13 wa Chad na wapiganaji 65 waliuawa katika makabiliano siku ya Ijumaa, kulingana na jeshi la Chad.

Serikali ya Chad imeahidi kutuma wanajeshi 2,000 kama sehemu ya kikosi cha Muungano wa Afrika kuunga mkono jeshi la Mali.

Rais Hollande alisema Jumamosi kuwa wanajeshi walipigana vikali na wapiganaji Kaskazini mwa nchi karibu na mpaka wa Algeria.

Makabiliano ya hivi karibuni kati ya wapiganaji wa kiisilamu na Tuareg katike eneo la Khalil, karibu na mji wa mpakani wa Tessalit.

Wapiganaji wa Tuareg wanataka kujitenga katika maeneo ya Sahara na Sahel, Mali, Libya, Algeria, Niger na Burkina Faso. Na wakati mmoja walikuwa wanashirikiana na wapiganaji wa kiisilamu lakini sasa wanaunga mkono wanajeshi wa Ufaransa.

Ufaransa ilipeleka wanajeshi 4,000 tangu mwezi Januari kusaidia serikali ya Mali kupambana na wapiganaji wa kiisilamu walikuwa wameyateka maeneo ya Kaskazini mwa nchi mwaka jana.