Muhtasari: Habari kuu leo Alhamisi

Miongoni mwa habari kuu leo, Rais Obama amemsifu Hillary Clinton na kuomba Wamarekani wampigia kura, mzozo unatokota kuhusu barua pepe za Clinton na Uturuki imefunga mashirika kadha ya habari.

1. Obama awaomba Wamarekani kumpigia kura Clinton

Haki miliki ya picha AFP

Rais Barack Obama amemuidhinisha Bi Hillary Clinton kuwania kiti cha Urais nchini Marekani, ili awe mwanamke wa kwanza nchini humo kuchukua hatamu za uongozi.

Akiongea huku umati mkubwa wa watu ukishangilia nderemo na vifijo, katika mkutano wa wajumbe wa chama cha Democtratic mjini Philadelphia, amempongeza kwa kuvunja dhana ya watu wengi dhidi ya wanawake, na kuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi hiyo, kuchaguliwa na chama kikuu cha kisiasa, kuwania kiti cha Urais.

Pia amemsifu kwa kuvunja vizingiti, kubuni na kupanua nafasi pamoja na fursa kwa Wamarekani wengi.

Awali seneta wa Virginia Tim Kaine, alikubali kuwa mteuzi wa chama hicho kuwania kiti cha naibu wa Rais.

2. Mvutano Marekani kuhusu barua pepe za Clinton

Haki miliki ya picha Reuters

Mvutano mkali umetokea kati ya vyama vikuu viwili vya kisiasa nchini Marekani, kile cha Democratic na wapinzani wao wa Republicans, kuhusiana na suala tata la barua pepe.

Kundi la Bi Hillary Clinton, limemshutumu mpinzani wake Donald Trump, kwa kuhujumu usalama wa taifa la Marekani.

Hayo yalianza baada ya Rais Barrack Obama, kusema kuwa huenda Urusi inamsaidia kisiri Bw Trump, kwa kudukua barua pepe inayoiaibisha uongozi wa chama cha Democratic.

Bw Trump, alijibu kwamba ingekuwa vyema Urusi ifanikiwe kuzipata na kufichua barua pepe 30,000 za Bi Clinton, zilizofutwa kutoka katika sava ya kibinafsi aliyotumia wakati alipokuwa akihudumu, kama waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani.

Uturuki yafunga mashirika ya habari

Haki miliki ya picha AFP

Wakuu nchini Uturuki wamefunga baadhi ya vyombo vya Habari katika juhudi za kuwasaka wahusika kwenye jaribio la mapinduzi iliyotibuka.

Magazeti 45 na runinga 16 yameamrishwa kufungwa mara moja.

Islamic State watoa video ya walioshambulia kanisa

Haki miliki ya picha AP

Kundi la Islamic State limeweka mtandaoni video inayo dhaniwa kuonyesha watu wawili wakimuuwa kasisi mmoja nchini Ufaransa ndani ya kanisa lake.

Mkanda huo wa video unaonyesha wakishikana mikono na kuapa kwa Kiarabu.

UN yalaumu kundi la Boko Haram

Haki miliki ya picha AP

Na Umoja wa Mataifa umelilaumu kundi lenye itikadi kali la Boko Haram, kwa kuhusika katika ghasia ambazo unasema hazieleweki iliyojaa ukatili na mauwaji nchini Nigeria.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja huo Stephen O'brien, amesema hatua za kundi hilo zimesababisha idadi kubwa ya watu kuyakimbia makaazi yao.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu milioni tisa wamevuka bonde la mto Chad na kuelekea maeneo mengine ya Nigeria, Niger, Chad na Cameroon kwa lengo la kutafuta msaada wa kibinadamu.