Arsenal yabanduliwa nje ya kombe la FA

Image caption Theo Walcot

Kwa mara nyingine matumaini ya klabu ya Arsenal, kumaliza ukame wa miaka zaidi ya saba ya bila kunyakuwa kikombe chochote yamepotea mchana wa leo,baada ya kupoteza mchezo wao wa marudiano dhidi ya klabu ya iliyoshuka daraja msimu uliopita, Blackburn Rovers.

Lilikuwa ni shuti kali la Martin Olsson's ambalo lilimshinda kipa wa Arsenal Wojciech Szczesny na kuzaa bao pekee lililofungwa na Colin Kazim-Richards kunako dakika ya 72 ya mchezo huo uliokuwa ukifanyika kwenye uwanja wa Emirates ndilo liliiwezesha Blackburn kuondoka na ushindi ugenini.

Arsenal wameshindwa kutwaa taji lolote kubwa kwa miaka zaidi ya saba,ambapo msimu huu wamekuwa na matumaini ya kufika mbali kwenye michuano ya kombe la FA jambo ambalo leo limeshindwa kutimia baada ya kuondolewa na Blackburn.

Mara ya mwisho Arsenal yenye maskani yake kaskazini mwa jiji la London,kutwaa kombe la FA ilikuwa mwaka 2005 na sasa wanakabiliwa na kibarua kingine mapema katikati mwa wiki hii wakati watakapokuwa wakiwakaribisha Buyern Munich kutoka Ujerumani katika mchezo wa 16 bora ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.

Matokeo ya leo yameifanya Arsenal kwa mara ya pili kuondolewa kwenye michuano mikubwa na klabu ndogo,ambapo mapema msimu huu waliondolewa kwenye Bradford kwenye kombe la ligi.

Kwenye msimamo wa ligi kuu soka nchini England,Arsenal wanakamata nafasi ya tano nyuma ya Tottenham wakiwa na point 44.